Tabia ya mtu inatokana na malezi aliyoyapata kwa kiasi kikubwa toka kwa wazazi,pia toka kwa walimu mashuleni, mafundisho ya dini,na toka kwa watu anaoonana nao na kuchangamana nao kila siku za maisha yake hasa wakati wa umri mdogo. Kulea watoto kulingana na tamaduni zetu katika karne hii ya teknolojia ni changamoto kubwa.
Watoto wa Dijitali ni wale ambao wamezaliwa katika karne hii ambayo teknolojia ya habari na mawasiliano imesomnga mbele sana kiasi ambacho taarifa zimekuwa nyingi kupita uwezo wakuzidadavua. Wazungu wanaita “Information Overload“.
Watoto hawa wa dijitali wanafahamu mambo mengi sana kuliko ambavyo wanatakiwa kufahamu katika umri husika jambo ambalo linaleta changamoto kubwa katika kulea watoto kwa wazazi wa zamani ambao walizaliwa kipindi ambapo teknolojia haikuwa katika kiwango hiki na mfumo wa malezi walioupata unatofautiana sana na wa sasa na pengine haufanyi kazi katika mazingira ya kisasa. Wazazi hawa nimewaita “Wazazi wa Analojia”.
Katika hali hii utakuta mtoto anafahamu mambo mengi tu ambayo wazazi hawayajui,ina maana mzazi anajifunza toka kwa mtoto,hii ina maana gani? Kuna madhara mara mbili
- Mzazi anakosa kujiamini katika jukumu lake la kumfundisha mtoto kwani anatambua sasa kuwa mtoto ni mjuaji wakati ungine kumzidi,na anaweza kuamua kutofanya hilo jukumu kwa kujua mtoto anafahamu tayari. Wakati mwingine inakuwa si sahihi.
- Mtoto anatambua baada ya muda kuwa mzazi wake hafahamu mambo mengi na kuwa yeye anafahamu zaidi. Hivyo naye anaacha kuuliza au kutaka kufahamu toka kwa wazazi. Hivyo anaweza akafanya vitu kwa ufahamu wake tu binafsi au kwa kutafuta msaada sehemu nyingine nje na wazazi wake. Na huenda msaada atakao pata ukawa sio sahihi.
Hali hii ni hatari katika ulezi wa watoto katika jamii yetu na ni lazima kuliangalia kwa mapana sana na kuchukua hatua stahiki.
No comments:
Post a Comment